UZINDUZI JUBILEI MIAKA 5O YA JIMBO

Tarehe 21/04/2021 siku ya jumatano, Jimbo Katoliki Singida limefanya uzinduzi wa Jubilei ya miaka 50. Itakumbukwa kuwa Jimbo hili lilianzishwa na kutangazwa na Baba Mtakatifu Paulo wa VI mnamo Machi 25, 1972 katika Sikukuu ya Kupashwa Habari Bikira Maria kuwa atakuwa mama wa Mungu na Malaika Gabrieli ambapo kilele cha maadhimisho hayo yatakuwa Agosti 21, 2022. Jimbo hili liliundwa kwa kuchukua sehemu za majimbo ya Mbulu, Dodoma na Tabora.

Akiongoza adhimisho la Misa Takatifu ya uzinduzi wa Jubilei hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, Mhashamu Bernard Mfumbusa, alisisitiza kusema kuwa; Jubilee ni kipindi cha sala na shukrani kwa Mungu kwa wema na ukarimu wake, na ni kipindi cha kujitathmini tulipotoka, tulipo na kuanza upya, kuwa na matumaini na kusamehe pale tulipokosea. “Msiogope kila kitu kinawezekana. Ni kipindi kizuri cha kujitathmini tunatoka wapi na tunaelekea wapi…Mungu akiwepo chochote kinawezekana.”

Akirejea kauli mbiu na salamu ya Jimbo Katoliki Singida inayosema Uhai Singida…Umoja na Mapendo, ambayo ni ya tangu mwaka 2008 wakati wa Jubilei ya miaka 100 ya uinjilishaji Jimboni Singida kipindi hicho ilisema; “Jubulei Singida…Umoja na Mapendo” na baada ya Jubilei ikwa; “Uhai Singida…Umoja na Mapendo, Mhashamu Askofu Mfumbsa alikaza kusema kuwa Umoja na Mapendo iwe ni tunu na dira muhimu katika Jubilei hiyo katika muktadha chanya wa kutangaza na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Jimbo, Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Mhashamu Edward Mapunda aliwashukuru wamisionari wote waliojisadaka na kushuhudia habari njema bila ya kujibakiza katika kipindi chote. Hata hivyo, Askofu Mapunda alihimiza waamini kushiriki kikamilifu mpango dira wa matukio yaliyoandaliwa kuelekea kilele cha Jubilei kwa kuiishi kauli mbiu ya Jimbo; “Uhai Singida…Umoja na Mapendo” ambapo kwa kipindi hiki cha Jubilei inakuwa; “Jubilei Singida…Umoja na Mapendo” ili kujiweka zaidi mikononi mwa Mungu na kumshukuru kwa zawadi ya Jimbo na Imani katika umoja na mapendo.

Matukio yaliyoambatana na adhimisho la uzinduzi wa Jubilei ni pamoja na kuwasha Mshumaa wa Jubilei, kubariki Msalaba utakaotembezwa kwenye parokia zote kipindi chote cha maadhimisho kuelekea kilele, na tukio la kurusha hewani “Njiwa wa Amani” kama ishara ya kusambaza amani, upendo na Habari Njema kwa mataifa.

Matukio mengine yatakayofanyaka katika mwaka huu wa jubilei ni pamoja na kusali novena, kufanya mafungo, kutoa semina mbalimbali juu ya maisha ya kiroho na kijamii, kufanya hija, matembezi ya Msalaba na mshumaa ambao ni ishara ya Kristo miongoni mwetu, kufanya matendo ya huruma na ukarimu, kuanzisha na kuimarisha vyama vya kitume, kuhamasisha miito ya utawa na upadre, kutoa katekesi endelevu na kutolewa msamaha kwa masuala mbalimbali ya kiroho-ikiwemo ubatizo.

Historia inaonyesha mafanikio makubwa sana yamepatika ndani ya Jimbo kwa kuangalia hali ilivyokuwa wakati linaanzishwa mpaka sasa. Jimbo lilianza likiwa na parokia 9, waamini 59,000, vingango zaidi ya 200, Mapadre 15 wa mashirika mbalimbali: Wapallotini, Damu Takatifu Ya Yes una Mapadre wa Mateso. Mapadre wazalendo walikuwa 4, kulikuwa na mashirika 3 ya masista yaani Medical Missionaries of Mary, Damu Azizi ya Yes una Masista wa Mtakatifu Gemma Galagni, makatekista 210. Kulikuwa na hospitali 1 tu ya Makiungu na Zahanati 4, seminari ndogo moja ya Dung’unyi ikiwa na waseminari 48, na waseminari 7 katika Seminari kuu. Mpaka kufika uzinduzi wa Jubilei Jimbo lina kuwa na Parokia 29, Waamini 186,797, Vigango zaidi ya 361, Makatekista 583, Mapadre wanajimbo waliopadrishwa 76 ambao kati yao ni Askofu wa sasa wa Jimbo hilo, Mhashamu Edward Mapunda. Mapadre wa Mashiriki wanayofanya kazi ndani ya Jimbo ni 32 ambapo kuna mashirika 30 ya kitawa ya kiume na kike. Mpaka sasa Jimbo la Singida limeongozwa kwa awamu tatu na maaskodu 3 (Askofu Bernard Mabula 1972-1999; Desiderius Rwoma 1999-2015, na Edward Mapunda 2015 mpaka sasa. Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa Mashirika ya watawa wa Kiume na kike, kudumisha huduma za kiafya ambapo kuna Hospitali 4, Vituo vya afya 3, Zahanati 9, huduma za elimu ambapo kuna Seminari ndogo 3, Sekondari 7 na Shule za Msingi 12. Jimbo pia mpaka sasa lina Vyuo 6, Kituo cha Kichungaji 1, Vituo vya walemavu na wazee 3, watoto yatima 1 sambamba huduma nyingine za kiroho na kijamii. Haya yote ni mafanikio ndani ya Jimbo.

Tuliombe neema na baraka za Mungu mafanikio zaidi na Jubilie yenye heri na fanaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *